WATU wengi walipigwa na butwaa na kubaki midomo wazi baada ya kuvuja kwa sauti inayodaiwa kuwa ni ya mchekeshaji Steve Mengere ‘Steve Nyerere’ na mama mzazi wa muigizaji Wema Sepetu.
Audio ilikuwa ya kawaida tu, lakini kilichofanya ionekane ishu, ni kule kuwahusisha watu wazito kwenye nchi hii na sakata la kukamatwa na baadaye kushtakiwa kwa matumizi ya bangi, kwa Wema. Kama ilivyotarajiwa, Steve Nyerere alitumia uungwana, akatoka mbele ya jamii na kuomba radhi.
Hicho ndicho kitu pekee ambacho alipaswa kukifanya, vinginevyo angekuwa mtu wa ajabu ‘kukausha’ ili kuacha upepo upite kama pepo zingine zinavyopita. Na niseme ukweli, utetezi wake pia nimeupenda, maana amesema kweli kuwa ilibidi atumie sanaa ili kumuweka vizuri mama ambaye aliishi naye vizuri kama mwanaye.
Ni vile tu mama Wema aliwahi kusema, lakini hata mimi nilikuwa najiuliza kwa kutomuona Steve akienda kumsabahi dada yake pale Central au hata kumsindikiza mahakamani. Historia inanionyesha huyu mchekeshaji huwa hakosi katika matukio yanayomhusisha Wema Sepetu na mara kadhaa, ameonekana akiwa karibu na mama Wema. Yes, ilibidi atumie sanaa ili kumuweka sawa na alifanikiwa.
Kwa hiyo, alichojaribu kusema ni kuwa yote aliyoongea ndani ya sauti ile, ni uongo. Kwamba hakwenda Dodoma, hakuongea na mawaziri waliotajwa wala wabunge na kwamba kilichotokea hakihusiani kwa namna yoyote na yeye. Lakini katika uhalisia wake, kuna uhusiano mkubwa wa kilichosikika na kilichotokea, ingawa siyo hoja ya leo hapa.
Ninachotaka tuwekane sawa, ni namna gani Steve Nyerere anapata mkate wake wa kila siku. Ukimsikiliza wakati akizungumza na waandishi wa habari, alisema yeye anaishi kwa sababu ya jina lake, alilotumia miaka mingi kulitengeneza. Steve ni muigizaji wa filamu na mchekeshaji. Huku kwenye filamu hajawahi kuwa staa wa kuuza sana kiasi cha kusema anaishi maisha tunayomuona kwa sababu hiyo.
Lakini pia kwenye uchekeshaji, siku hizi kuna kitu kinaitwa Stand Up Comedy, ile ambayo msanii anawajaza watu ukumbini na yeye kuanza kuwachekesha. Wanafanya hivi pia waigizaji wengine ambao kwa Afrika Mashariki, kinara wao ni Eric Omondi wa Kenya, Anna Kasiime wa Uganda na hapa nyumbani, MC Pilipili pia hufanya. Siku hizi Steve Nyerere naye anafanya Stand Up Comedy.
Ni kwa kiasi gani Stand Up Comedy ya Steve inamuingizia hela ni jambo la kujadili. Steve anaishi sababu ya jina lake kwa kufanya kazi za sanaa au anaishi kisanii? Kuna uwezekano mkubwa pia kwamba licha ya sanaa, Steve anaishi kisanii, ndiyo maana sanaa aliyosema aliitumia katika kumuweka sawa mama Wema, inafanana sana na maisha yake halisi.
Steve anafika sehemu ambazo wengi hawawezi kufika na anazungumza na watu ambao siyo kila msanii anaweza kuwafikia. Watu wote waliotajwa katika ile sauti wanaweza kufikiwa na huyu msanii bila matatizo yoyote, ingawa zipo pia chumvi za kutosha katika hilo.
Unashangaa kumuona Steve Nyerere akipanda katika jukwaa la muziki na kuanza kumtunza mwimbaji manoti mengi mithili ya wale mapedeshee tuliowazoea, kina Chief Kiumbe, Papaa Msofe, Muzamir Katunzi, Jack Pemba, Ndama Mutoto ya Ng’ombe na wengine wa aina hiyo.
Kutoa ni moyo na si utajiri, lakini ni kweli kijana wa Kitanzania anayepata hela kwa jasho lake kihalali, anaweza kugawa fedha nyingi kwenye starehe kama Steve anavyofanya? Ingawa siungi mkono hata kidogo kitendo kilichofanywa na Mama Wema, ni vyema nikamtahadharisha Steve kwamba kilichotokea halikuwa jambo la bahati mbaya. Yale ndiyo maisha yake, ya kutumia sanaa yake.
Na huenda siyo kwa mama Wema pekee, sanaa hiyo yaweza kuwa imetumika ‘kuwaweka’ sawa pia watu kibao ambao hatuwafahamu!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni