Dar es Salaam. Matumaini ya Watanzania kupata mgawo wa sukari yanazidi kufifia baada ya msako wa wafanyabiashara walioficha bidhaa hiyo kuchukua sura mpya kila uchwao.
Msako huo unaoendeshwa na maofisa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana na polisi, ulianza baada ya Rais John Magufuli kutoa agizo hilo wiki iliyopita. Hata hivyo, licha ya kukamatwa sukari inayodaiwa kufichwa, imebainika kuwa baadhi ya waliohifadhi hawakuwa wameificha, bali walikuwa wanakamilisha taratibu za kodi na vibali.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara hao waliokuwa wanadaiwa kuficha zaidi ya tani 5,000, wamepewa ruksa ya kusambaza sukari hiyo na kuiuza kwa bei elekezi.
Miongoni hao ni Al-Neem Abdul Zacharia mwenye kampuni ya Al-Neem, ambaye kontena zake 70 zenye tani 1,840 za sukari zilidhaniwa kuwa zimefichwa bandarini.
Lakini jana, ilibainika kuwa taratibu za kutoa kontena hizo bandarini zilikuwa hazijakamilika.
Meneja wa kampuni hiyo, Zacharia Haroon alisema sukari hiyo ilinunuliwa Februari kutoka kwa kampuni ya Zenj General Traders na kibali kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kilipatikana juzi.
“Ilikuwa inasafirishwa Burundi lakini tukaomba tuinunue kwa sababu ya upungufu wa sukari hapa kwetu,” alisema.
Haroon ambaye ni baba wa mmiliki wa kampuni hiyo, alisema baada ya mwezi mmoja, kontena za sukari zilifika katika Bandari ya Dar es Salaam na taratibu za malipo ya kodi na kupewa kibali zilichukua muda mrefu ndiyo maana kontena hizo ziliendelea kubaki bandarini hadi walipopata kibali cha Serikali Mei 5 na cha TFDA juzi.
Alisema kwa sababu taratibu hizo zimekamilika sukari hiyo itaanza kusambazwa kwa wauzaji. “…Itauzwa kwa bei elekezi (Sh1,800),” alisema Haroon.
Maofisa wa Takukuru ambao wameagiza sukari hiyo isambazwe kwa wauzaji ndani ya saa 36, walisema kati ya kontena hizo, 30 zilikuwa katika Bandari ya Dar es Salaam na 40 katika bandari kavu ya Ubungo.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi, Takukuru, Leonard Mtalai alisema walianza kufanyia uchunguzi taarifa za kuwapo kwa sukari hiyo baada ya chanzo chao kuwaeleza kuwa sukari hiyo ni mali ya Mbunge wa Mpendae Salim, Turky. Hata hivyo, Turky alisema hausiki na sukari hiyo.
Vilevile, sukari nyingine tani 4,900 iliyokuwa imekamatwa Mbagala imerejeshwa kwa mmiliki wake kwa ajili ya kuisambaza.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema sukari hiyo imeachiwa kwa sababu mfanyabiashara huyo awali hakuwa amekamilisha baadhi ya taratibu, sasa zimekamilika.
Alisema kwa kipindi hicho, sukari ilikuwa kwenye maghala chini ya forodha.
“Amekamilisha taratibu za kodi, kibali cha Bodi ya Sukari na TFDA mwishoni mwa wiki,” alisema Kayombo na kuongeza kuwa baada ya kukamilisha taratibu hizo ametakiwa kuanza kusambaza sukari yake na kuuza kwa bei elekezi.
Serikali yaagiza tani 70,000
Serikali imeanza kupokea sukari kutoka nje, ikiwa ni sehemu ya tani 70,000 ilizoagiza ili kukabiliana na uhaba uliopo huku ikiwataka wasambazaji kuiuza kwa Sh1,800.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ilisema jana kuwa tayari tani 11,957 zimeshawasili nchini na zitaanza kusambazwa leo kwenye mikoa yote.
Majaliwa ambaye aliondoka jana kwenda London, Uingereza kumwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa mapambano dhidi ya rushwa, alibainisha kuwa kutoka kwenye mzigo huo; tani 2,000 zitapelekwa mikoa ya Kaskazini, 3,000 Kanda ya Ziwa, 2,000 mikoa ya Kusini, tani 2,000 zitaelekezwa Nyanda za Juu Kusini. Mikoa ya Kanda ya Kati itapata tani 2, 000.
Alisema tani nyingine 24,000 zitawasili Ijumaa na kuanza kusambazwa kuanzia Jumatatu ijayo na mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Juni, Serikali itapokea tani nyingine 20,000.
Akamatwa na kilo 4,000
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam imekamata kilo 4,000 za sukari ilizosema zimefichwa katika eneo la Hananasif, Kinondoni mali ya Bushir Haroun.
Baada ya kukamatwa Haroun alisema: “Naona mmeniwahi, maana nilipanga leo kuitoa msaada katika kuelekea miezi ya Shaaban na mwezi Mtukufu wa Ramadhan.”